Vijana wasiopungua 45,000 watakaomaliza kidato cha sita watajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na watakaokwepa mafunzo hayo ya miezi mitatu, watashtakiwa.
Mpango huo wa kupitisha JKT wahitimu wa kidato cha sita na vyuo, ambao ulifutwa mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na matatizo ya kifedha na kurejeshwa bila mafanikio ya miaka ya hivi karibuni, ulilenga kujenga uzalendo kwa vijana na kuongeza ukakamavu.
Jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk Hussein Mwinyi alisema utaratibu huo ni wa kisheria na si hiari, hivyo wahitimu wa kidato cha sita watambue kuwa ni kosa kukaidi wito wa kujiunga na JKT.
Dk Mwinyi, aliyekuwa anawasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, vijana watakaojiunga na jeshi watafanya hivyo kwa awamu tatu.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha vijana 20,000 ambao wataingia katika mafunzo hayo Juni hadi Septemba 2014 na kufuatiwa na wa awamu ya pili itakayochukua vijana 14,450 kuanzia Oktoba hadi Januari 2015 wakati awamu ya tatu ya vijana 10,550 itaanza Januari hadi Aprili 2015.
Hata hivyo, kumekuwepo na mwingiliano wa muda wa kujiunga na jeshi hilo na wa kujiunga na masomo ya juu. Kati ya vijana 15,000 waliotakiwa kujiunga na jeshi hilo kati ya Oktoba 2013 na Januari 2014, waliojiunga walikuwa 1,002 tu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano huo, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alisema atatoa ufafanuzi huo leo.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alitaka mafunzo ya JKT kwa wabunge yafanyike kwa miezi miwili hadi mitatu badala ya wiki mbili.
Bulaya, ambaye alipitia mafunzo hayo pamoja na wabunge wenzake wakati mpango huo uliporejeshwa mapema mwaka jana, alisema kuwa hali hiyo itawafanya wabunge hao kujifunza mambo mengi zaidi.
Bulaya aliwataja baadhi ya wabunge vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa ni John Mnyika (Chadema-Ubungo) na Catherine Magige (viti maalumu-CCM).
“Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu wabunge kwenda kwenye mafunzo kwa miezi miwili hadi mitatu,” alisema na Bulaya na kuongeza:
“Katika kambi za JKT kuna tatizo la vifaa vya afya, hivyo wizara iliangalie hilo ili wanaokwenda katika mafunzo hayo wapate tiba sahihi na kwa wakati.”
Wataka muda uongezwe
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuhusu wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Vita Kawawa alipendekeza muda wa JKT uongezwe hadi miezi sita.
Kawawa alisema ingawa Serikali inasema kuongeza muda huo kunashindikana kutokana na mabadiliko ya mihula ya masomo vyuoni, bado wanasisitiza umuhimu wa kuongeza muda wa mafunzo.
Kamati hiyo imeshauri vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na JKT na wale ambao hawataripoti kwa mafunzo bila sababu za msingi, Serikali iwachukulie hatua za kisheria.
Bajeti ya Wizara
Kuhusu bajeti, Dk Mwinyi alisema wizara yake itatumia Sh1.26 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali, zikiwamo kununua ndege za kivita.
Dk Mwinyi aliliambia bunge kuwa kati ya Sh1.26 trilioni, Sh1.0 trilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati kiasi cha Sh249 bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa na wizara hiyo ni pamoja na kununua vifaa na zana za kijeshi, ikiwamo vifaa vya uhandisi wa medani na ndege za kivita.
Pia,alisema wizara itaanza ujenzi wa gati katika Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Kigamboni, kuboresha mifumo ya mawasiliano ya ndani na nje ya vikosi vya kambi za jeshi na kuendelea na ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya wanajeshi.
Dk Mwinyi alizitaja shughuli nyingine zitakazofanywa kuwa ni kukamilisha ujenzi wa shule ya mafunzo ya awali ya kijeshi (RTS), eneo la Kihangaiko, Pwani na Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC), Tengeru Arusha.
Pia,wizara itaanza ujenzi wa hospitali kuu ya jeshi eneo la Mataya mkoani Pwani, kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za kijeshi na pia kulipa madeni ya kimkataba.
Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema kuwa pamoja na bunge kuidhinishia wizara hiyo Sh1.1 trilioni kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka huu, hadi Machi ilikuwa imepokea Sh768.4 bilioni, sawa na asilimia 69.7.
Sign up here with your email