Utajiri wa Nay, Umaskini wa Mr. T-Touch

IKIWA humfahamu kwa sura mkali wa midundo Bongo, Thabith Mango ‘Mr. T-Touch’ ni lazima utakuwa unafahamu kazi zake hata kwa kuzisikia tu zikichezwa kwenye vituo mbalimbali vya redio au mitaani.

Baadhi ya kazi hizo ni Muziki Gani, Salamu, Akadumba zote alizofanya na Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Too Much ya Darasa, Angejua na Komela za Dyna Nyange, Chafu Pozi wa Bill Nas na Jike Shupa wa Nuh Mziwanda.

Mr. T-Touch alianza kufahamika zaidi kupitia Studio ya Sedactive kwa kutengeneza ngoma kali lakini umaarufu ulikolea zaidi baada ya kupiga kazi nyingi na mkali Nay wa Mitego zilizowafanya kuwa washikaji wakubwa waliotengeneza ‘chemistry’ kali katika Muziki wa Bongo Fleva.



Nay na Mr. T- Touch kwa sasa hawaivi, wamepata ‘ajali ya kisanaa’, katika makala haya T amefunguka mambo mengi kuhusu ugomvi wao:

BMM: Umeanza kufanya kazi na Nay wa Mitego lini?

Mr. T- Touch: Muda mrefu umepita, zaidi ya miaka mitano.

BMM: Nini hasa ilikuwa siri ya ushikaji wenu?

Mr. T-Touch: Nafikiri damu tu ziliendana hasa baada ya kuwa tunatengeneza chemistry nzuri kwenye kazi zetu. Unajua mimi ndiye nimemfanya Nay kufika hapo alipo japo sina kitu, nina mchango wa kama asilimia 80 kwenye mafanikio yake akatae ama akubali!

BMM: Unasema una mchango mkubwa kwenye mafanikio yake, vipi kuhusu mafanikio yako wewe tangu umeanza kufanya naye kazi, amewahi kukulipa?

Mr. T-Touch: Sina mafanikio kabisa zaidi ya kuwa na studio yangu mwenyewe. Mwanzoni nilipokuwa nafanya kazi na Nay tulikuwa tunafanya kazi kishikaji na hajawahi kunilipa hata shilingi 10. Makubaliano yalikuwa kulipana kwenye matamasha na mauzo ya nyimbo, lakini hilo hakuwahi kulitekeleza. Hata hivyo, sikuona shida kwa sababu nilikuwa naangalia fursa, kwamba kupitia kumng’arisha mshikaji ningeweza kufanya naye kazi zingine kama kuandaa matamasha yangu na yeye kunisapoti!

BMM: Umewahi kuandaa tamasha halafu ukaomba sapoti yake lakini hakufanya hivyo?

Mr. T-Touch: Ndiyo, tena juzikati tu hata miezi miwili haijamalizika. Niliandaa tamasha mkoani lililonigharimu kama milioni moja hivi, mshikaji tulikubaliana kwamba atatokea kwenye tamasha hilo lakini mwisho wa siku hakutokea. Nikapata hasara, nilipomuuliza kwa nini alinifanyia hivyo hakuwa na jibu lolote la kunipa!

BMM: Umesema umefungua studio yako mwenyewe iitwayo Touch Sound, studio uliyopewa na Nay kama zawadi (Free Nation) vipi mlipokosana ulirudisha kila kitu kwake?

Mr. T-Touch: Kama nilivyotangulia kusema awali, kila kitu mimi na Nay tulikuwa tunafanya kishikaji, kwa hiyo hata hiyo Studio ya Free Nation japo alijitapa kwenye media kuwa alinipa kama zawadi lakini ukweli ni kwamba ilikuwa ni yake na mimi ni kama nilikuwa namfanyia kazi yeye.

BMM: Lakini chini ya kapeti kwenye sababu za kutengana kwenu kuna mambo mengi yanatajwa, hebu funguka sababu hasa!

Mr. T-Touch: Tumeshindwa kwenda tu sawa kimasilahi, hakuna zaidi, nahitaji mafanikio kwa sasa.

BMM: Umewahi kugombana na Nay kwa ishu yoyote ile huko nyuma?

Mr. T-Touch: Yap, kuna kipindi alitaka kurekodi na mimi sikuwa sawa. Nilipomwambia akadai nimemdharau, tulizinguana kiasi kwamba akaamua kuchukua vifaa vyake vya studio, lakini baadaye tuliweka mambo sawa.

BMM: Kuna chochote unamdai baada ya kuondoka kwenye studio yake?

Mr. T-Touch: Kuhusu studio simdai chochote, lakini namdai pesa kama shilingi milioni moja kwa ishu zingine ambapo siwezi kuziweka wazi hapa.

BMM: Mara ya mwisho kuzungumza naye ni lini?

Mr. T-Touch: Nilipoondoka kwenye studio yake, Julai 30, mwaka huu.

Nay anasemaje?

Kwa upande wa Nay akimzungumzia Mr. Touch amenukuliwa akisema mshikaji huyo kwake ni kama mtoto anayetakiwa kutoka nyumbani na kwenda kujitafutia. Hana ubaya naye na ikitokea kukawepo na sababu ya kufanya kazi hakuna ubaya wowote
Previous
Next Post »

Blogger templates