FAHAMU KAMA MPENZI WAKO ANAKUPENDA KWA KUANGALIA YAFUATAYO


Naam! ninaongea na wanaume ambao wanapenda kufahamu kama wenzi wao wanawapenda kwa dhati. Rafiki zangu mnajua mapenzi ni kama mchezo wa kujificha na kutafutana? Yaani hauna kanuni maalum, unaweza kukimbilia huku lakini mwenzako akahangaika sehemu nyingine akikusaka!

Ingekuwa hisia ni rahisi kama sauti, basi mtu angesimama juu ya mlima mrefu na kupiga kelele lakini si hivyo. Ni mchezo unaohitaji mbinu nyingi, umakini wa hali ya juu na utulivu uwanjani! Hautaki papara.

Wengi leo hii wapo kwenye uhusiano ambao hawana uhakika nao, utakuta mtu yupo na mwanamke ambaye hajui kama anampenda kama anavyompenda yeye au lah! Hilo ni tatizo, maana unaweza kuendelea kupoteza muda wako kwa siku nyingi, lakini mwisho akakutosa na kukuacha vibaya ukiwa bado hujajiandaa kuachwa!

Ipo mifano mingi, nimeongea na wengi kwenye simu na hata ana kwa ana, kilio chao ni hicho hicho, wametendwa na wenzi wao ambao wamekuwa nao kwa muda mrefu sana wakiamini kwamba wanawapenda kumbe ni kinyume chake.

Mbaya zaidi ni kwamba wakati wakiachwa wanakuwa tayari wameshawagharamia vitu vingi vya thamani, fedha n.k, hapo unakuwa mwanzo wa kuchanganyikiwa na kuharibu kila kitu katika maisha yao! Naam...sasa nakupa mbinu muhimu zaidi zilizopendekezwa na wataamu wa Saikolojia ya Mapenzi, zitakazoweza kukusaidia kutambua kama mwanamke uliyenaye ana mapezi ya kweli kwako.

Zipo ishara ambazo mwanamke akizifanya utaweza kufahamu ameegemea upande gani katika penzi lenu! Hapa chini ni baadhi ya ishara unazotakiwa kuziangalia unapokuwa na mwanamke katika mahusiano (hasa nyakati za mwanzoni) kabla hujaamua kuingia kichwa kichwa. Hebu tuzione.

KUJITOA KWA KILA HALI
Kama mwanamke anakupenda kwa dhati, atajitoa kwako kwa kila hali. Unajua, kuna mambo ambayo si rahisi kufanyiwa na kila mtu, yapo ambayo yanafanywa kwa watu wanaopendana tu. Huyu atajitoa kwako.

Atafanya mambo muhimu ambayo si rahisi kuyafanya kwa mtu mwingine. Anatakiwa kukupa vipaumbele kwenye mambo yake yote. Kwa kukueleza mipango yake (hata ile ya siri) na kukufanya wa kwanza kujua kinachoendelea katika maisha yake.

Lazima ujiulize na uangalie, je, wewe ni moja ya vipaumbele vyake? Je, wewe unakuwa wa kwanza kujua mambo yake kabla ya rafiki zake? Je, uzito anaochukulia kwako ukiwa na tatizo, ndiyo anaouchukua pia kwa rafiki zake ama ndugu zake? Lazima kuwe na tofauti. Siku zote, umuhimu wako hauwezi kuwa sawa na mfanyakazi mwenzake ofisini.

Mwanamke wa aina hii, ni rahisi kukuambia: “Nachukia jinsi kaka yangu anavyompiga mdogo wetu wa mwisho. Ni tabia mbaya inayonikosesha usingizi.” Unaweza kuona ni jambo dogo, lakini fahamu kwamba amekufanya rafiki na kukueleza mambo ya ndani kabisa ya familia yake. Anafanya hivyo kwasababu anakuamini, anajua wewe ni yeye na yeye ni wewe! Upo rafiki yangu? Hebu tuone kipengele kingine hapa chini...

WASIWASI NA USALAMA WAKO
Baadhi ya wanawake wanaweza kusema mengi lakini wasiwasi kwa ajili ya usalama wa mtu unayempenda ni muhimu sana. Hii ni moja ya njia ya kujua kama mwanamke anakupenda. Anapenda kujua uko wapi, unafanya nini na utarudi nyumbani muda gani?



Si rahisi kufanya hivyo kwa mwanaume ambaye hana mapenzi naye. Anafanya kwako, kwasababu anakupenda na anajali usalama wa maisha yako, na si maisha yako pekee, bali kuna jambo kubwa na zito zaidi; ANAJALI USALAMA WA PENZI LAKE maana hataki kukupoteza na kulipoteza penzi hilo!

WIVU
Ingawa si lazima awe na wivu lakini inaelezwa kwamba wivu ni moja ya alama ambazo unatakiwa kuziangalia wakati ukimchunguza kama anakupenda kwa dhati. Wivu ni ladha ya mapenzi. Ni kama ndimu kwenye mchuzi au kitunguu swaumu kwenye pilau! Unaonaeeeh?!
Wivu ni afya ya uhusiano, kwamba lazima aoneshe wasiwasi na wewe, atilie mashaka simu yako, achunguze email yako, blog na hata ukurasa wako wa Facebook! Hana nia mbaya, lakini anachotaka kujua, ni kweli yupo peke yake?
Previous
Next Post »

Blogger templates