Wastara Juma ataka kujiua kwa sumu….Kisa chadaiwa ni madeni, manyanyaso na kutongozwa mara kwa mara na wanaume

IKIWA imetimia mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu kifo cha mumewe, Juma Kilowoko ‘Sajuki’, staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma, Jumamosi iliyopita amedaiwa kufanya jaribio la kutaka kujiua kwa kunywa sumu….
KABLA YA YOTE
Awali, staa huyo ambaye amepitia mitihani mingi, alitundika picha katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram na kulalamika kuumwa tumbo.
 
Katika maelezo aliyoyaandika sambamba na picha hiyo, Wastara alimshukuru msanii mwenzake, Tamrina Poshi ‘Amanda’ kwa msaada aliompatia kwa kuwa alikuwa katika hali mbaya.
 
SUMU YATAJWA
Siku chache baada ya kuweka picha hiyo, Risasi Mchanganyiko lilipata kisa kizima kupitia kwa chanzo chake makini kuwa staa huyo alisumbuliwa na maumivu ya tumbo baada ya kuokolewa katika jaribio lake la kutaka kukatisha uhai wake kwa kunywa sumu.
 
SUMU ILIYOTUMIKA
Inadawa kuwa Wastara aliamua kunywa vidonge aina ya fragile kwa kuchanganya na pombe kwa lengo la kukatisha uhai wake ili kuondokana na manyanyaso anayoyapa kutoka kwa baadhi ya watu.
 
HAUSIGELI AOKOA JAHAZI
Inadaiwa kuwa wakati staa huyo akiwa chumbani kwa lengo la kujiua, msaidizi wa kazi ‘hausigeli’ aliingia chumbani humo kwa nia ya kufanya usafi ndipo alipomkuta Wastara akiwa analia huku amejiinamia.
 
“Hausigeli alijaribu kumuuliza sababu ya kilio chake lakini Wastara hakumjibu kitu, aliendelea kulia bila kikomo,” kilisema chanzo hicho.
 
Inadaiwa kuwa baada ya kutojibiwa kitu, hausigeli huyo alitoka na kumfuata Amanda ambaye alikuwa katika chumba kingine na kumweleza hali aliyomkuta nayo Wastara chumbani humo.
 
AMANDA APATWA NA MSHTUKO
Baada ya kuingia chumbani kwa Wastara, Amanda alipatwa na mshtuko mkubwa alipomkuta shoga’ke akiwa na baadhi ya vidonge mkononi na kumuuliza kisa cha kutaka kumeza vidonge hivyo.
 
“Wastara alimwongopea Amanda kwamba vidonge hivyo ni kwa ajili ya kujitibia mguu wake lakini Amanda hakukubaliana na maelezo hayo baada ya kuiona chupa ya bia iliyokuwa pembeni, kwa kuwa anafahamu Wastara siyo mnywaji wa pombe, ndipo  alipobaini lengo lake la kutaka kujiua,” chanzo kiliendelea kushusha data hizo.
 

Chanzo hicho kimesema kuwa Amanda alimpatia huduma ya kwanza shoga’ake huyo kwa kumnunulia maziwa na kumpeleka katika dispensari ya karibu ili kupata matibabu zaidi ya kuondoa sumu ya vidonge alivyovimeza.
 
SABABU ZA KUTAKA KUJIUA
Kwa mujibu wa chanzo kingine cha habari, Wastara alitaka kukatisha uhai wake kutokana na kuchoka kunyanyapaliwa, kudhalilishwa na kutongozwa mara kwa mara na wanaume, hali ambayo imekuwa ikimfedhehesha mbele ya jamii.
 
Chanzo hicho kimesema kwamba kabla ya tukio hilo, Wastara alikuwa akilalamika kudhalilishwa na watu anaowadai fedha zake ambao hawataki kumlipa haki yake.
 
“Kuna watu wengi ambao Wastara anawadai lakini wanamsumbua kwa kumuona ni mwanamke asiye na nguvu na wengine wanatumia mwanya huo kumtongoza, mwenyewe anaamini haya yote yanatokea kwa kuwa Sajuki hayupo,” kimetoboa chanzo hicho.
 
Habari zaidi zinadai kwamba hivi sasa Amanda anaendelea kumwekea ulinzi wa karibu Wastara ili asiweze kuchukua uamuzi mbaya wa kukatisha maisha yake. Source: Gaeti la  Risasi Mchanganyiko/ GPL
Previous
Next Post »

Blogger templates