Gari hilo linalomilikiwa na pedeshee maarufu Bongo, Mohammed Kiumbe ‘Chief Kiumbe’ limewekwa sokoni baada ya staa huyo kuchemsha kutoa fedha za kulinunua pamoja na kupewa muda wa kufanya hivyo.
Awali, iliripotiwa kuwa gari hilo ni mali ya Diamond ambaye alikuwa akitamba nalo kila pembe ya Jiji la Dar huku akijinasibu kwamba amelishalipa fedha za kutosha kwa ‘Big Boss’, Chief Kiumbe.
Wengi waliamini na kumweka Diamond au Sukari ya Warembo katika matawi ya juu kutokana na kumiliki gari hilo lenye thamani kubwa na lililojaa vikorombwezo vingi ndani yake.
Picha za Diamond akiwa ndani ya gari hilo zilionekana kwenye magazeti huku akikaririwa kwamba analimiliki kihalali gari hilo aina ya Toyota Landcruiser V8 lenye thamani ya shilingi milioni mia moja na laki moja (100,100,000).
Siku chache zilizopita, Chief Kiumbe alimnyang’anya Diamond gari hilo kwa kile kilichodaiwa kuwa staa huyo alishindwa kutoa ‘mpunga’ wa kulinunua pamoja na kukaa nalo kwa muda mrefu.
Baada ya hapo gari hilo likapotea machoni mwa watu kwa kutojulikana lilipokuwa limefichwa ingawaje ilidaiwa kuwa Chief Kiumbe alikuwa ameliweka stoo.
Mapaparazi wa Risasi Mchanganyiko walilitafuta gari hilo kwa udi na uvumba, ndipo walipobaini kwamba lilikuwa limewekwa sokoni katika yadi moja iliyopo maeneo ya Kijitonyama, Dar likipigwa bei.
Waandishi wetu walifika katika yadi hiyo na kujifanya wanunuzi na kuambiwa kuwa gari hilo lilimshinda Diamond.
“Hili gari lina vitu vingi vizuri, ukiwa na ‘sensa’ ndipo unapoweza kuondoka nalo kwa sababu halitumii funguo, bila hivyo huwezi, Diamond ameshindwa kulinunua,” alisema jamaa aliyekutwa katika yadi hiyo.
Waandishi hao walitajiwa bei na kupewa nafasi ya kulikagua gari hilo kila kona, hatimaye waliondoka ndani ya yadi hiyo wakiahidi kurudi na mkwanja ili kufanya kile kilichomshinda Sukari ya Warembo.
Sign up here with your email