WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amenusurika kifo
hivi karibuni baada ya ndege ya shirika la Precision Air, iliyokuwa
ikitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kupata hitilafu ya injini.
Ndege hiyo, ambayo iliondoka Mwanza saa 2:30 usiku, ilipata
hitilafu ya injini moja muda mfupi tu baada ya kuruka, hali
iliyomlazimu rubani wa ndege hiyo kubadili mwelekeo na
kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akizungumza na Mtanzania jana, Sumaye, ambaye alikuwa
mmoja wa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo, alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo.
Sumaye alisema kitendo cha injini kupata hitilafu, ilimlazimu
rubani wa ndege hiyo kuruka na injini moja mpaka KIA,
ambako walitafutiwa ndege nyingine ili kuendelea na safari.
Alisema kutokana na tatizo hilo, abiria walilazimika
kuondoka KIA kwa kugawanywa kwenye ndege tofauti
zilizokuwa zikielekea Dar es Salaam ambapo Sumaye
aliondoka saa 7 kasoro usiku.
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA), Bestina Magutu, alipotafutwa ili kujua
kilichotokea kwenye ndege hiyo, alisema kuwa
hakuwa na taarifa zozote za hitilafu ya ndege hiyo.
“Hebu ongea nao wenyewe, sijapata taarifa zozote
mpaka sasa, nimetoka ofisini jana sikuwa na taarifa,”
alisema Magutu.
Naye Mratibu wa Masoko wa Precision Air, Hilaly
Mremi, alipozungumza na Mtanzania alikiri kutokea
kwa hitilafu hiyo ya ndege.
“Kwa kifupi hakuna ajali iliyotokea, hitilafu
zinazotokea kwenye ndege ni za kawaida
kama ambavyo gari inaweza kuharibika
na kupakiwa pembeni,” alisema Mremi.
Alisema safari za shirika hilo zinaendelea kama kawaida
na kutaja namba ya ndege hiyo kuwa ni TW 415.
Ndani ya wiki hii, ndege mbili za shirika hilo zimenusurika
ajali baada ya kupata hitilafu wakati zikiwa angani.
Mbali na ndege hiyo aliyokuwemo Sumaye, ndege nyingine
ya shirika hilo yenye namba ya safari Pw 77 na ya usajili TWC,
iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda Kilimanjaro ilinusurika kupata
ajali juzi jioni na hivyo kulazimika kurudi na kutua kwa dharura
uwanjani hapo baada ya kupata hitilafu ikiwa angani.
Mbali na Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
naye aliwahi pia kupata ajali mwaka jana akiwa kwenye ndege za
shirika hilo.
Lowassa alikuwa miongoni mwa abiria 37 waliokuwa wamesafiri
na ndege hiyo ambayo ilipasuka magurudumu manne ilipokuwa
ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Katika ndege hiyo pia kulikuwa na maofisa mbalimbali wa Serikali
na Jeshi la Wananchi, ambao walikwenda kuhudhuria sherehe
ya kutolewa kamisheni kwa maofisa wa jeshi katika Chuo cha
Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA).
Sign up here with your email