Luis Suarez abakishwa kifungoni

image


Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imeunga mkono uamuzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wa kumfungia mshambuliaji wa Uruguay na Barcelona, Luis Suarez kucheza soka kwa miezi mine.Katika uamuzi wake uliotolewa leo, Suarez aliyetiwa hatiani kwa kumng’ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini, ataruhusiwa kufanya mazoezi na pia kucheza mechi za kirafiki, ikiwamo mechi ya Jumatatu hii dhidi ya Club Leon ya Mexico.Wanasheria wa Suarez walidai kortini kwamba uamuzi wa Fifa kumzuia kushiriki shughuli zozote zinazohusu michezo mshambuliaji huyo aliyehama Liverpool kiangazi hiki ilikuwa adhabu ya kupitiliza. CAS imesema itatoa ufafanuzi juu ya sababu za uamuzi wake huo
baadaye.Kutokana na uamuzi huo, Suarez sasa anaweza kushuka dimbani katika mechi ya kwanza ya kiushindani Oktoba 26 mwaka huu wakati Barcelona watakapocheza na Real Madrid. Umoja wa Kimataifa wa Wachezaji (Fifpro) umeeleza kusikitishwa kwake kwa CAS kushikilia marufuku ya miaka mine kwa mchezaji huyo.

Suarez aliyesajiliwa kwa pauni milioni 75 na bado hajatambulishwa Nou Camp, ataendelea kutumikia kukosa mechi tisa za kimataifa, lakini anaweza kwenda kwenye mechi zozote kama mtazamaji na kushiriki shughuli za promosheni.
CAS ilisema katika taarifa yake kwamba kimsingi adhabu zilizotolewa na Fifa dhidi ya mchezaji huyo zimeidhibishwa isipokuwa tofauti hizo ndogo. Ikasema kumzuia kufanya mazoezi kumepitiliza na kutamwathiri katika kazi yake baada ya muda wa kifungo kumalizika.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Suarez kung’ata mchezaji uwanjani, na jana Ofisa Mtendaji wa Ligi Kuu ya England, Richard Scudamore alisema Suarez ni ajali inayosubiri kutokea wakati wote na kwamba hakusikitishwa kuondoka kwake England.
Suarez ndiye mchezaji bora na mfungaji bora kwa England msimu uliopita, lakini aliharibu mambo kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil kwa kuendeleza tabia yake ya kung’ata kana kwamba ni mumiani.
Scudamore amesema pamoja na matatizo yake yote, Suarez anabaki kuwa mchezaji mzuri na mwenye kipaji cha hali ya juu wala hawezi kumpokonya sifa yoyote.
Katika tukio jingine, rufaa ya klabu ya Legia Warsaw ya Poland dhidi ya Celtic ya Uskochi kutaka warejeshwe kwenye hatua za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imetupwa na Bodi ya Rufaa ya Uefa.
Legia walitolewa kwa kuchezesha mchezaji ambaye alikuwa na kadi nyekundu, ambapo licha ya kuwafunga Celtic jumla ya mabao 6-1 kwenye mechi mbili, wamepoteza nafasi muhimu waliyopigania kwa muda mrefu. Legia sasa wamepanga kupeleka rufaa yao CAS
Previous
Next Post »

Blogger templates