Jinsi Inde ilivyomfuta machozi Dully Sykes

Dully Sykes anasherehekea mafanikio ya wimbo wake ‘Inde’ aliomshirikisha kijana wa WCB, Harmonize.

      
Na hakika mkongwe huyu miaka ya hivi karibuni alikuwa akijaribu kurudi tena kileleni lakini wapi! aliachia miradi mingi kama vile Shuka na Tuachie aliyowashirikisha vijana wa Yamoto Band lakini zote zilidunda!
Hizo ni nyimbo mbili tu kati ya nyingi za miaka ya hivi karibuni alizitoa Dully na zote zikashindwa kuyabariki masikio ya mashabiki wa muziki. Kiukweli, mkongwe unapotoa nyimbo nyingi na zote zikaishia kuchezwa mara mbili tatu kwenye TV na redio kisha kutupwa kapuni, ni lazima ujitathmini kuona wapi unakosea hadi iwe hivyo.
Na kwa wasanii wengine, kukataa tamaa huwa kitu cha kwanza kuwakabili. Kwa Dully Sykes, kufanya production kumekuwa kimbilio lake pindi muziki wake unapoangukia pua. Lakini kiukweli, muziki bado ulikuwa ukimdai Dully Sykes na kumvuta shati kila muda kumtaka asiugeukie mgongo.
Kama ambavyo atafutae hapaswi kuchoka, Dully alimjumuisha Harmonize kwenye wimbo wake mpya, Inde, ambao rasmi umeuondoa mkosi aliokuwa nao. Mapokezi ya Inde yamekuwa vile ambavyo neno la Kiingereza ‘overwhelming’ linaweza kuubeba uzito wa kilichotokea.
Inde umekuwa Inde kweli. Madada na makaka, kutwa wamekuwa wakijipost Instagram wakiimba goma hilo. Haijawahi kutokea kwa Dully katika kipindi cha miaka mingi – kuwa na wimbo uliopokelewa kwa uzito huo.
Tayari video yake, imetazamwa kwa zaidi ya mara milioni 1, wiki chache tu tangu utoke. Hajawahi kuwa na namba kama hizo katika video zake zote alizowahi kuzitoa. Video yake inachezwa Trace TV karibu kila leo – hajawahi kuwa na video iliyopokelewa hivyo na vituo vya nje.
Kwanini? Kizuri chajiuza. Inde ni wimbo mkali ukilinganisha na nyimbo nyingi alizotoa hivi karibuni. Mtaani wimbo huo unalia kila kona. Hilo halijatokea kama bahati tu, ni kwasababu Inde ni wimbo tofauti na zile Dully amekuwa akizitoa hivi karibuni hasa alizotayarisha mwenyewe.
Na kiukweli, nimewahi kupenda nyimbo zake chache tu alizotengeneza mwenyewe. Sababu hasa ni kuwa amekuwa na midundo yenye kufanana sana na isiyokuwa na kitu kipya masikioni. Pengine Inde imempa fundisho kuwa, iwapo anataka kuendelea kuwa muimbaji yule tuliyemfahamu kupitia hits zake kama ‘Baby Candy’ na zingine, anapaswa kuwapisha watayarishaji wengine wamtengenezee.
Kama atapenda kuendelea kutengeneza nyimbo zake, basi afanye kwa uchache sana ama ahusike tu kwenye ukamilishaji wake tu.
Previous
Next Post »

Blogger templates