WANAFUNZI WATUPWA JELA MIAKA 6 KWA MAUAJI YA MWALIMU WAO MKOANI SINGIDA



Vijana wawili waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chemchem wilayani
 Mkalama katika Mkoa wa Singida, wamehukumiwa kifungo cha miaka sita kila
 mmoja baada ya Mahakama kuwatia hatiani kwa kosa la mauaji ya mwalimu wao.

Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma inayoendesha vikao vyake mjini Singida, ilitoa
 hukumu hiyo jana.
Waliohukumiwa ni Shani Mtua na Mohammed Salimu ambao  wakati walipotenda
 kosa hilo, mwaka 2008,  walikuwa Kidato cha Tatu na walikuwa na umri wa miaka
 18 kila mmoja.
Ilielezwa mahakamani kwamba kulikuwa na washitakiwa wengine wawili katika kes
i hiyo; Emmanuel Daud na Michael Msengi, walikufa wakiwa mahabusu  wakisubiri
 kesi yao kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Hukumu  ilitolewa na Jaji Rehema Mkuye baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka
 la kuua bila kukusudia walilofanya katika Kijiji cha Mpambala,  Tarafa ya Kirumi 
Wilaya ya Mkalama.
Awali, Mwanasheria wa Serikali,  Zakaria Elisaria aliyekuwa anasaidiwa na Karen 
Mrango, alidai mahakamani kwamba washitakiwa walihusika na mauaji ya  Rajabu
 Idude (49), aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu shuleni hapo. Ilidaiwa walifanya mauaji 
hayo  Agosti 2008.
Mwanasheria huyo wa Serikali alidai chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa 
kwanza , Shani, kupewa barua ya kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kutokana
 na utovu wa nidhamu na kisha akashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu huyo.
Zakaria alisema wanafunzi hao walimvizia mwalimu huyo katika kichaka cha karibu na
 shule yao wakampiga ngumi na mateke, kisha wakamjeruhi mwilini kwa kisu alichokuwa
 nacho mshitakiwa wa kwanza.
Inadaiwa kutokana na kipigo hicho,  Mwalimu Idude alipiga kelele na mwanawe 
aliyetajwa kwa jina la Maye Rajabu,  alifika haraka kwenye eneo la tukio, lakini 
akakuta ameshakufa.
Wanafunzi hao (washitakiwa) hawakukutwa katika eneo hilo lakini msako ulifanyika
 usiku huo na wanafunzi wanne walikamatwa. Baada ya kuhojiwa kuanzia ngazi ya
 mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani, walikiri kosa.
Kwa upande wake, Wakili wa washitakiwa, kutoka Kampuni ya Uwakili ya  Kim & 
Company, Raymond Kimu, alimwomba Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu dhidi ya wateja
 wake, kutokana na kuonesha ushirikiano  wa kutosha tangu siku waliyokamatwa.
Aidha, alidai washitakiwa walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri mdogo
 wa utoto. Alidai  ni wakosaji wa mara ya kwanza, wanajutia kosa hilo na kwamba 
wamekaa jela kwa muda mrefu wa miaka sita, hivyo wamejifunza kutokana na mauaji hayo.
Akitoa hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna ubishi kwa yote aliyosema wakili wa utetezi
. Hata hivyo alisema, anadhani sababu hizo siyo kibali kwa washitakiwa hao kupanga na 
kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao aliyekuwa anasimamia nidhamu.
“Nadhani kosa walilofanya haliwezi kukubalika kwa  jamii hata kidogo…fujo zimekuwa
 zikitokea kwenye mashule na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi cha kuathiri utendaji…
, kufuatia kosa hili, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka sita jela,” alisema Jaji Mkuye
Previous
Next Post »

Blogger templates